Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM yaomba ufadhili zaidi kuwasaidia wakimbizi wa Syria Lebanon

UN Photo/Paulo Filgueiras
Ross Mountain, Mratibu wa Hahaki za Binadamu. Picha@

UM yaomba ufadhili zaidi kuwasaidia wakimbizi wa Syria Lebanon

Idadi ya wakimbizi wa Syria nchini Lebanon inaongezeka kwa kasi zaidi ya uwezo wa jamii ya kimataifa kuchangia fedha za kukidhi mahitaji yao yanayoongezeka, amesema Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Ross Mountain.

Bwana Mountain amesema wakimbizi wapya wa Syria wapatao 12,000 wanaingia Lebanon kila wiki, huku idadi nzima ikitarajiwa kufikia milioni 1.5 mwishoni mwa mwaka, ambayo ni thuluthi moja ya idadi nzima ya watu nchini humo.

Akizungumza mjini Geneva, Bwana Mountain amesema wengi wa wakimbizi wa Syria wanapewa hifadhi na jamii maskini nchini Lebanon, na ushindani kuhusu rasilmali zinazoendelea kupunguka unaweza kuzua utata baina ya wakimbizi na wenyeji wao. Amesema kufikia sasa, ombi la dola bilioni 1.6 kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Syria walioko Lebanon, limepokea mchango wa dola milioni 500 pekee.

“Kuwaweka pamoja Walebanon maskini zaidi na Wasyria maskini, kwani Wasyria wakipokea angaa riziki kutoka kwa UNHCR na wadau wengine huku Walebanon hawapati usaidizi huo kwa sasa, ni njia moja ya kudhoofisha usalama na kuleta mzozano. Tayari takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 37 ya idadi nzima ya wafungwa Lebanon ni raia wa Syria. Nitajaribu kuwahimiza wadau wa ufadhili kuwa hili si tu tatizo la kibinadamu. Hili ni tatizo linalohitaji watu kuwaza kuhusu utulivu wa nchi na ukanda mzima."

Zaidi ya wakmbizi milioni 1.1 wa Syria wameandikishwa nchini Lebanon.