Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani shambulizi dhidi ya makao makuu ya serikali Somalia

UM walaani shambulizi dhidi ya makao makuu ya serikali Somalia

Mwakilishi wa Katibu Mkuu na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nichola Kay, amelaani shambulizi lililofanywa jana usiku dhidi ya Villa Somalia, ambayo ni makao makuu ya serikali ya Somalia mjini Mogadishu.

Shambulizi hilo ni miongoni mwa msururu wa mashambulizi yanayotekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab dhidi ya taasisi za kisiasa nchini Somalia, na limetokea baada ya jingine lililojaribiwa kufanywa mnamo tarehe 5 Julai.

Akizungumza leo baada ya kukutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu Abdiweli Sheikh Ahmed, Bwana Kay amesema maendeleo ya kisiasa nchini humo yanawezekana tu kupitia taasisi za kisiasa, na ndio maana zinashambuliwa na wale wanaojaribu kuitumbukiza tena Somalia katika migogoro. Ameahidi uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa watu na taasisi za Somalia katika ujenzi wa amani na utulivu.