Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika ya Mashariki zapambana na biashara haramu ya mbao

Picha: UNEP

Nchi za Afrika ya Mashariki zapambana na biashara haramu ya mbao

Wakati mkutano wa  kwanza wa baraza la mazingira UNEA ukiendelea mjini Nairobi, serikali za Kenya, Uganda na Tanzania zimetangaza kuanzisha mradi mpya wa pamoja ili kupambana na biashara haramu ya mbao, kwa ushirikiano na mashirika ya Umoja wa Mataifa na INTERPOL.

Akizungumza na Watangazaji wa Redio ya Umoja wa Mataifa huko Nairobi, David Mbugua, mkurugenzi wa idara ya Misitu Kenya, amesema mkakati huo mpya utasaidia kudhibiti usafirishaji wa mbao katika ukanda mzima na kuhakikisha utumiaji endelevu wa rasilimali.

Ameongeza kwamba, angependela kuona nchi zingine zikiungana na mradi huo, hasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo kiasi kikubwa cha biashara haramu kinafanyika, na pia nchi ambazo zinapokea mbao hizo kama vile nchi za Uarabuni.

Raisi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, John Ashe, amepongeza harakati hizo katika hotuba yake mbele ya UNEA, akisema jitihada hizo za kutunza mazingira si chaguo tu bali ni hatua ya lazima kwa sisi sote.