Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel yatakiwa kutopitisha sheria ya kushinikiza mlo kwa waliogoma kula

Juan Mendez. (Picha@UN /Mark Garten)

Israel yatakiwa kutopitisha sheria ya kushinikiza mlo kwa waliogoma kula

Mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya utesaji wa haki za kiafya, amelitaka Bunge la Israel kusitisha mpango wake wa kufanyia marekebisho sheria ya wafungwa ambayo itoa mwanya kwa dola kuwalazimisha wafungwa walioko kwenye mgomo wa kula kuachana na mgomo huo.

Wito wa mjumbe huyo Juan Mendez umekuja katika wakati ambapo Bunge la Israel likihairisha kwa mara ya pili upigiwaji kura kwa mswaada huo ambao unataka kubadilisha sheria za magereza kwa kupiga marafuku kitendo cha mfungwa kuendesha mgomo wa kutokula pindi awapo gerezani.

Kumekuwa na mamia ya wafungwa wa Kipalestina ambao wapo kwenye mgomo wa kula nchini Israel na iwapo marekebisho hayo yakapitishwa basi wafungwa hao huenda wakaandamwa na sheria hiyo mpya.

Wafungwa hao waliokuwa kwenye mgomo huo tangu Aprili 24 mwaka huu, wanalalamika kitengo cha kuendelea kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

Akizungumzia zaidi kuhusu hatua inayokusudiwa kuchukuliwa na Bunge la Israel Mendez amesema kuwa kitendo cha kumlazimisha mfungwa kula wakati akiwa gerezani hakikubaliki hata kidogo.

Amelitaka bunge hilo kutobadilisha sheria hiyo akisema kuwa hatua hiyo ni uvunjifu wa haki za binadamu.