Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nusu ya raia wa Yemen waathirika na njaa: WFP

Watoto wa kike watalengwa na miradi ya WFP Yemen ili waweze kwenda shuleni. @WFP/Micah Albert

Nusu ya raia wa Yemen waathirika na njaa: WFP

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP, limetangaza leo kuwa nchini Yemen, zaidi ya watu milioni 10, sawa na nusu ya raia wote wa nchi hii, wameathirika na njaa. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte

Kwa Mujibu wa WFP, watu milioni 5 wako hatarini kukumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula. Msemaji wa WFP, Elisabeth Byrs, amesema:

“ Milioni 5 ni idadi kubwa sana. Kwa hiyo tumepanga kuongeza msaada wetu, hasa kwa watoto, kwa sababu, Yemen ina kiwango cha juu zaidi duniani cha utapiamlo wa watoto. Nchini humo, nusu ya watoto chini ya miaka mitano, yaani milioni 2, wamechelewa kukuwa kwa sababu ya ukosefu wa chakula, na milioni moja ya watoto wameugua utapiamlo”.

Amesema WFP hivi sasa linatoa msaada wa chakula maalum kwa watoto hao pamoja na wajawazito na wanaonyonyesha. Chakula hicho ni pamoja na supu yenye vitamini na lishe ya soya.

Miradi mingine itakayoanzishwa kwanzia mwezi wa Julai italenga kuwawezesha raia wa Yemen kupata suluhu za kudumu kwa ukosefu wa usalama wa chakula, kupitia kilimo, ajira, upatikanaji wa maji na chakula shuleni kwa wasichana.

Msemaji huyo amesema pia kwamba hali ya usalama Yemen ni mbaya sana, lakini hata hivo, WFP imeweza kufikia watu kupitia vituo 3600 vya usambazaji wa chakula.

WFP limeeleza kwenye ripoti yake kuwa hali hiyo mbaya ya ukosefu wa usalama wa chakula imesababishwa pia na kutegemea sana chakula kutoka nje, kwani Yemen inaingiza asilimia 90 ya mahitaji yake ya chakula, hasa ngano na sukari, kwa hiyo nchi hii inakumbwa sana na mabadiliko ya bei za vyakula kwenye soko la kimataifa.