Siku ya Walinda Amani, ubunifu na teknolojia katika kuimarisha usalama: Ashe

29 Mei 2014

Leo ikiwa ni Siku ya Kimataifa ya Walinda Amani, rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, John W. Ashe, amesema ni lazima kuhakikisha kuwa changamoto za kiusalama katika nchi walinda amani wanakotoa huduma zao zimeshughulikiwa, ili kuweka mustakhbali endelevu kwa wote katika jamii ya kimataifa.

Akitoa wito wa kuwaenzi walinda amani kwa changamoto na hatari wanazokumbana nazo kila siku kwa ajili ya amani, Bwana Ashe amehimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wadau wa kijamii na wengineo kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni: “Ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa: Vikosi vya Amani. Vikosi vya Mabadiliko. Vikosi vya Mustakhbali mwema.”

Bwana Ashe amesema ulinzi wa amani bado ni rasilmali muhimu katika uhifadhi wa amani na usalama wa kimataifa, na kwamba ufanisi wake unategemea uhusika na ushirikiano endelevu baina ya Baraza la Usalama, Baraza Kuu, Sekritatariati ya Umoja wa Mataifa, pamoja na nchi wanachama zinazochangia walinzi wa amani na rasilmali za kifedha.

Rais wa Baraza Kuu amesema zaidi ya walinda amani 111,000 wanahudumu katika maeneo 16 ambayo ni hatari zaidi duniani, na kwamba wakati huu wa kuandaa jukwaa la ajenda ya maendeleo baada ya 2015, ubunifu, teknolojia, na hususan teknohama mpya itachangia zaidi katika kuimarisha usalama wa kimataifa.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter