Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urusi yatumia kura turufu kupinga azimio la kuipeleka Syria ICC; Yatoa sababu, Marekani yazungumza

Wakati wa kikao cha May 22 cha Baraza la Usalama (Picha ya UM/Eskinder Debebe)

Urusi yatumia kura turufu kupinga azimio la kuipeleka Syria ICC; Yatoa sababu, Marekani yazungumza

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeshindwa kupitisha azimio la kuipeleka kesi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita nchini Syria kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Nchi kumi na tatu wanachama wa Baraza hilo zimeunga mkono mswada wa azimio hilo, lakini kwa sababu ulipingwa na Urusi, mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, huku Uchina ikionyesha kutoegemea upande wowote, mswada huo haukupitishwa.

Kufuatia hatua hiyo, Marekani kupitia mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Samantha Power ikaeleza..

(Sauti ya Balozi Samantha)

Kwa masikitiko makubwa, kutokana na uamuzi wa Urusi wa kuungano mkono Serikali ya Syria kwa lolote lile ifanyalo, wananchi wa Syria hawatapata haki hii leo. Watashuhudia uhalifu lakini si adhabu.”

Alipopata fursa ya kutoa taarifa yake, mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Vitaly Churkin akatanabaisha..

 (Sauti ya Balozi wa Urusi)

Rasimu ya azimio iliyokataliwa leo inadhihirisha azma ya kutumia ICC kufanikisha matamanio ya kisiasa na kuweka misingi hatimaye ya kuwezesha shambulio la kijeshi. Inapaswa kueleweka kuwa hii ripoti ya Ceaser inayoibua mvutano na kutumika kwenye utangulizi wa rasimu hii ilitokana na taarifa zisizothibitishwa kutoka kwa vyanzo visivyothibithwa na hivyo haiwezi kutumiwa kupitisha uamuzi huo mkubwa.”

Mapema kabla ya kura hiyo, ujumbe wa Katibu Mkuu kwa Baraza la Usalama ulisisitiza kuwa uwajibikaji kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaweza kuzuia ukatili zaidi nchini Syria. Ujumbe wa Bwana Ban umesomwa na Naibu wake Jan Eliasson kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

(JAN ELIASSON)

"Tangu kuibuka kwa mzozo Syria, nimerejea mara kwa mara umuhimu wa uwajibikaji kwa wahusika wa uhalifu huu mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu, uhalifu dhidi ya binadamu na hata wa kivita. Mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu na watendaji, ambayo yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita, yanaongeza udharura wa kuchukua hatua sasa za uwajibikaji Syria."