Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya watoto Jamhuri ya Afrika ya Kati inazidi kuwa tete: UNICEF

@MINUSCA

Hali ya watoto Jamhuri ya Afrika ya Kati inazidi kuwa tete: UNICEF

Mzozo unaoendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR unahatarisha sana hali ya watoto nchini humo, amesema mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo Souleymane Diabaté.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari mjini New York, Marekani Diabate, amesema ingawa hali ya nchi ilikuwa mbaya sana kabla mkurupuko wa vita, hivi sasa imeongezeka zaidi.

Kwa mujibu wa UNICEF, kila dakika 21, mtoto moja anafariki dunia CAR kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuiliwa. Amesisitiza wasiwasi wake juu ya hali ya watoto.

“ Watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanashuhudia ghasia mbaya sana. Unawaangalia machoni, na unaona kwamba wamepotea. Ni kama ndoto mbaya, lakini ni ukweli unaotokezea. Mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati umesahaulika, na jamii nzima ya nchi hiyo imeathirika na mzozo huo, wakiwemo watoto”.

Alieleza pia kuwa watoto 6000 wamejtumikishwa kwenye vikundi vilivyojihami na amesema, licha ya hali mbaya ya usalama nchini humo, UNICEF itaendelea kuwapatia watoto huduma za chanjo, hasa za polio, kutekeleza mradi unaoitwa “rejelea shuleni” kwa ajili ya watoto waliotumikishwa jeshini, na kusambaza chakula maalum kwa watoto walioathirika na utapiamlo.