Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lamulika silaha za maangamizi

Naibu Katibu Mkuu wa UM Jan Eliasson akihutubia Baraza la usalama kuhusu silaha za maangamizi. (Picha:UN/ Evan Schneider)

Baraza la usalama lamulika silaha za maangamizi

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu kuzuia kusambaa kwa silaha za maangamizi ikiwa ni miaka 10 tangu kupitishwa kwa azimio la kupinga silaha hizo. Ripoti ya Alice Kariuki inafafanua zaidi.

(Ripoti ya Alice)

Nchi 20 bado hazijaridhia azimio la kudhibiti silaha za maangamizi na tunazisihi zifanye hivyo kwani mara nyingi magaidi hutumia upenyo huo kulenga nchi zenye udhibiti hafifu, amesema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson katika hotuba yake ya ufunguzi kwenye mjadala huo. Amesema hakuna uhalali wowote wa matumizi ya silaha hizo na kila mtu ana wajibu wa kuzuia upatikanaji au matumizi ya silaha hizo.

(Sauti ya Eliasson)

“Sote tuna maslahi na wajibu wa kuzuia watu binafsi na vikundi visivyo vya kiserikali kupata na kutumia silaha hizi za kuchukiza. Hakuna mikono salama kwa silaha zisizo sahihi.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini Yun Byung aliongoza kikao hicho akatoa angalizo kuhusu kitisho cha Korea Kaskazini cha kutaka kufanya jaribio lingile la nne la nyuklia..

(Sauti ya Yun)

“Iwapo Korea Kaskazini itafanikiwa kupata silaha za nyuklia itahatarisha kabisa mkataba wa udhibiti wa nyukli, na utachochea mvutano na ukosefu wa utulivu Kaskazini-Mashariki mwa Asia. Jitihada za pamoja za kimataifa zitumike kuzuia majaribio zaidi ya nyuklia ya Korea Kaskazini.”

Baraza la usalama limeridhia taarifa ya Rais wa Baraza la Usalama linalohusu kuzuia kuenea kwa silaha za maangamizi S/PRSC/2014/7.

Azimio 1540 la mwaka 2004 linataka nchi kujiepusha kusaidia kwa njia yoyote ile kutengeneza, kununua au kusafirisha silaha za nyuklia, kikemikali au kibaiolojia.