Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya usafi wa mikono duniani yamulika wahudumu wa afya:WHO

Usafi wa mikono

Siku ya usafi wa mikono duniani yamulika wahudumu wa afya:WHO

Tarehe 5 Mei kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kunawa mikono ambapo shirika la afya duniani WHO mwaka huu limeamua kuangazia wahudumu wa afya kwani kitendo cha baadhi yao kuhudumia wagonjwa bila kutakasa mikono yao husababisha vifo vya wagonjwa 30 katika kila wagonjwa 100.

WHO inasema magonjwa yanayohusiana na maambukizi hospitalini hutokea pindi vijidudu vinapohamishwa na mikono ya mhudumu wa afya anapohudumiwa wagonjwa. Kiwango cha uambukizi ni wagonjwa Saba kati ya 100 kwa nchi za kipato cha juu na wagonjwa 10 kati ya 100 kwa nchi za vipato vya chini na kati.

Shirika hilo linasema wagonjwa wanapoambukizwa vijidudu visivyotibika vyema kwa viua vijisumu au antibiotics, hupata madhara makubwa zaidi na gharama kubwa na kuna uwezekano wakafariki dunia kuliko wagonjwa wengine.

Limetaja kijidudu sugu kwa dawa hizo kiitwacho MRSA ambacho kiwango cha uambukizi ni asilimia 44 Amerika Kusini, asilimia 40 Afrika Magharibi na asilimia 38 barani Ulaya.

Kwa mantiki hiyo WHO kupitia afisa wake Bernadetta mjini Geneva anatoa wito.

(Sauti ya Bernadetta)

Bila hatua leo hakuna tiba kesho hakikisha maeneo makuu matano ya WHO ni sehemu ya kumkinga mgonjwa wako dhidi ya vijidudu sugu.”

Maeneo hayo ni kabla ya kumshika mgonjwa, kabla ya taratibu yoyote ya kitabibu, baada ya kugusa majimaji kutoka mwa mgonjwa, baaada ya kumgusa mgonjwa na baada ya kugusa mazingira alimokuwemo mgonjwa.