Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Polio pori yatishia mafanikio ya kutokomeza polio duniani: WHO

Mtoto akipokea chanjo dhidi ya polio

Polio pori yatishia mafanikio ya kutokomeza polio duniani: WHO

Shirika la afya duniani, WHO limetoa mwongozo wa muda utakaowezesha nchi zinazokabiliwa na ugonjwa wa polio pori kuweza kuchukua hatua ili kuondoa hatari ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huo duniani wakati huu ambapo msimu wa uambukizi unaanza. Taarifa zaidi na Alice Kariuki.

(Taarifa ya Alice)

Mwongozo huo unatokana na kikao cha kamati ya dharura kuhusu kanuni za afya kimataifa kilichofanyika tarehe 28 na 29 mwezi uliopita huko Geneva, Uswisi.

Kamati ilisema mwelekeo wa sasa wa kuenea kwa polio pori unahatarisha mafanikio ya kutokomeza polio duniani, ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kwa chanjo.

Imesema hadi mwishoni mwa mwaka jana asilimia 60 ya visa vya polio vilitokana na kuenea kwa Polio Pori na kuna ushahidi ya kwamba wasafiri watu wazima ndio wanaosababisha uambukizo huo.

Nchi zilizotajwa kukumbwa na Polio pori ni Somalia, Nigeria, Cameroon, Afghanistan, Equatorial Guinea, Ethiopia, Israel, Pakistan na Syria. Dkt. Bruce Aylward ni Mkurugenzi Mkuu Msaidizi WHO anazungumzia mapendekezo hayo ya muda.

(Sauti ya Dkt. Bruce)

WHO imetaka nchi yoyote ambayo kwa sasa haina polio itakapobaini uwepo wa ugonjwa huo, isingatie mwongozo uliotolewa huku ikisihi wadau wa shirika hilo kusaidia nchi kutekeleza mwongozo huo.