Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni lazima mianya wanayotumia magaidi kusafiri izibwe: CTED

Ni lazima mianya wanayotumia magaidi kusafiri izibwe: CTED

Msaidizi wa Katibu Mkuu ambaye pia Mkurugenzi Kamati ya Kukabiliana na Ugaidi, CTED, Jean Paul Laborde, amesema magaidi hutumia mianya iliyopo mipakani kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine, na kwamba ni lazima mianya hiyo izibwe ili kufanikisha juhudi za kupiga vita ugaidi.

Bwana Laborde amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, leo, ambako yeye na maafisa wa polisi ya kimataifa, Interpol, na Shirika la Usafiri wa Angani, ICAO wamezungumza. Laborde amesema vitambulisho vya usafiri na ulinzi wa stakabadhi za usafiri vinaweza kusaidia katika kuhakikisha magaidi hawasafiri kwa urahisi, huku akitaja vitu vingine vinavyochangia usafiri wao kwa urahisi

Sauti ya Laborde

Magaidi hawaheshimu mipaka. Mipaka yenye mianya hurahisishia magaidi kuvuka kutoka nchi moja hadi nyingine. Pia mafunzo duni na uhaba wa vifaa kwa maafisa wa usalama na maafisa wa forodha katika nchi nyingi. Siku hizi magaidi wanatumia stakbadhi bandia kusafiri, wanazipata kwa njia ya udanganyifu, au kubadilisha zilizo halali. Mianya hii pia inatumiwa na wahalifu wengine. Ni lazima tuizibe mianya hii.”

Bwana Laborde ameorodhesha baadhi ya mambo yanayotakiwa kufanywa kuhakikisha mianya wanayotumia magaidi kusafiri inazibwa

(Laborde )

Kwanza, udhibiti thabiti wa mpiaka ni nguzo muhimu ya kukabiliana na ugaidi. Pili, nchi wanachama zizuie usafiri wa magaidi kwa kuhakikisha kuwa mipaka, vitambulisho na stakbadhi za usafiri zinadhibitiwa vyema. Tatu, nchi wanachama zina vifaa kadhaa vinavyoweza kutumiwa, kama vile mfumo wa vitambulisho vilivyopotea na kupatikana vya Interpol na programu ya ICAO ya utambulisho wa usafiri.”