Mary Robinson atembelea jimbo la Kivu Kusini na kuonyesha mshikamano na wananchi

9 Aprili 2014

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi za maziwa makuu Afrika, Mary Robinson amefanya ziara yake ya kwanza kabisa kwenye eneo la Bukavu, lililoko jimbo la Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako amekuwa na mazungumzo na mamlaka husika na makundi mbali mbali.

Ziara hiyo ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mpango wa amani, usalama na ushirikiano uliotiwa saini mwaka jana huko Addis Ababa na nchi 11 wa Ukanda huo.

Mathalani alikutana na Gavana wa Bukavu Cisihambo na kujadili umuhimu wa kuimarisha usalama kwa kuondoa makundi yaliyojihami na kuyajumuisha kwenye jamii na hivyo kutekeleza mpango wa DDR.

Halikadhalika amesisitiza umuhimu wa kujikita zaidi katika miradi ya maendeleo ili harakati za kuleta amani ziwe na mtazamo chanya kwa maisha ya wakazi wa jimbo hilo la Kivu Kusini.

Bi. Robinson pia alikuwa na mazungumzo na viongozi wa Umoja wa Mataiaf na makundi ya wanawake ambapo alionyesha mshikamano nao hasa alipotembelea hospitali ya Penzi na kukutana na wanawake wahanga wa ukatili wa kingono.