Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna matumaini ya Kisiasa Haiti, Kipindupindu kinadhibitiwa: UM

Kuna matumaini ya Kisiasa Haiti, Kipindupindu kinadhibitiwa: UM

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limejulishwa kuhusu hatua muhimu zinazoendelea nchini Haiti zinazoimarisha harakati za uchaguzi baadaye mwaka huu.

Wajumbe wamesikiliza ripoti ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyosomwa na mwakilishi wake maalum nchini humo Sandra Honoré ambaye amesema maridhiano ya hivi karibuni baina ya jamii tofauti yamewezesha kutiwa saini kwa makubaliano ya El Rancho tarehe 14 mwezi huu.

Amesema mashauriano baina ya serikali, bunge na vyama vya siasa yalikuwa ni ya aina yake katika historia ya Haiti na kwamba kitendo hicho kinapaswa kuimarishwa kupitia mchakato wa kidemokrasia, utawala wa kisheria na uongozi bora pamoja na kukidhi mahitaji muhimu ya jamii.

Bi. Honoré amesma kwa ujumla kuna utulivu kiasi lakini kuna umuhimu wa kuimarisha jeshi la polisi nchini humo wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa umejiondoa katika vitengo saba vya kijeshi na kutoa fursa zaidi kwa Haiti.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhutubia Baraza la Usalama, Bi. Honoré ameulizwa kuhusu hali ya Kipindupindu kilichozuka nchini Haiti Oktoba mwaka 2010.

(Sauti ya Bi. Honoré)

“Kwa hali ilivyo sasa kwa ujumla visa vya ugonjwa vimepungua kwa asilimia 50 na kiwango cha vifo ni chini ya asilimia Moja, kiwango ambacho kwa mujibu wa WHO ni cha kuanza kutoa hadhari mapema. Kati ya visa 680,820 vilivyoripotiwa ugonjwa uliolipuka 2010, ni asilimia Sita tu ya kiwango hicho kiliripotiwa mwaka 2013, ikilinganishwa na asilimia 51 mwaka 2011. Hii inaonyesha kuwa kuna maendeleo katika kukabiliana na kipindupindu nchini Haiti.”

Bi. Honoré amesema Umoja wa Mataifa umeandaa mpango wa usaidizi wa miaka miwili wenye thamani ya dola Milioni 68 kwa ajili ya kusaidia mpango wa miaka 10 wa serikali ya Haiti wa kutokomeza kipindupindu.