Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la FAO Tunis laangazia uboreshaji wa kilimo

Kongamano la FAO Tunis laangazia uboreshaji wa kilimo

Shirika la Chakula na Kilimo duniani, FAO, limewaomba viongozi wa Afrika wahamasishe uwekezaji katika sekta ya kilimo ili kuondoa njaa barani humo.Ombi hilo limetolewa katika Mkutano wa 28 wa  ukanda wa Afrika, mjini Tunis, Tunisia ambao umeanza Jumatatu.

Afrika ndilo bara ambalo bado linatatizika katika kukabiliana na njaa, ukosefu wa chakula na vipato vidogo vijijini, kwa mujibu wa FAO, ingawa uchumi wa bara hili unakua kwa kasi.

Naibu Mkurugenzi wa FAO Kanda ya Afrika Bukar Tijani, amesema kwamba nchi Saba kati ya 10 zinazoendelea kwa kasi kubwa zaidi duniani ziko Afrika, kwa hiyo changamoto ni kutumia ukuaji huo kuwezesha wakulima wadogo na kusaidia uwekezaji, na kubadilisha mfumo wa kilimo kuwa  na uzalishaji mkubwa zaidi.

FAO inasisitiza kwamba kuna haja ya kushindana na mazao yanayoingizwa toka nje, kuendeleza masoko ya ndani, na biashara za kilimo, hasa biashara ndogondogo na zile zinazohusika na upatikanaji wa chakula mijini.

Tijani amesema kinachohitajika zaidi kufikia uzalishaji bora ni kupatikana kwa mikopo, pembejeo, huduma mbalimbali vijijini na kutumia teknolojia mpya.

Ametaja mifano mbalimbali ya mafanikio ya kilimo bora, ikiwemo kupata aina bora za ndizi Afrika Mashariki na Kati, kubaini aina za mbegu za mahindi zinazoleta mavuno bora zaidi, kuimarisha uzalishaji wa chai au maua Afrika ya Mashariki.

Hata hivyo Tijani amezungumzia hatua ya kuchukua kuongeza tija..

(Sauti ya Tijani)

 “Inabidi tuvutie vijana katika kazi za kilimo, kwasababu mpaka sasa hivi wanafikiria kilimo ni shughuli ya zamani, ya utamaduni, na hawajakiona kama biashara, au kazi ya kujiendeleza kiuchumi. Lakini vijana wanapaswa kuingia kwenye shughuli za kilimo, kwa sababu ni biashara kubwa hivi sasa duniani. Kwa hiyo  kongamano hilo litaangalia jinsi gani vijana wataweza kushirikishwa ili wafaidike na kilimo, ambayo ni sekta inayoleta faida kubwa kifedha hivi sasa.”

Kongamano hilo linatoa kipaumbele kwa vijana, ambao wanaweza kutegemea kilimo, uvuaji, au ufugaji kwa kupata ajira na kipato.