Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi na wenyeji wagombea rasilimali Sudan Kusini, UNHCR yatiwa hofu

Wakimbizi na wenyeji wagombea rasilimali Sudan Kusini, UNHCR yatiwa hofu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema lina hofu kubwa juu ya ghasia mpya zinazoibuka kutokana na uhaba wa chakula na maeneo ya malisho huko eneo la Maban jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

UNHCR inasema kumeibuka mvutano kwenye eneo hilo kati ya wakazi na wakimbizi na wanachogombania ni rasilimali ikiwemo chakula, kuni na eneo la malisho ya wanyama. Mvutano huo umesababisha mapigano ya hivi karibuni na wakazi wa eneo hilo la Maban wanataka wakimbizi Elfu Sitini wanaoishi kwenye kambi mbili waondoke ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.

UNHCR inasema inashirikiana na mamlaka husika huko Maban na wadau wengine wa usaidizi wa kibinadamu kupunguza mvutano huo wakati huu ambapo wakimbizi Elfu Nane wamelazimishwa kuondoka kambini. Fatoumata Lejeune-Kaba ni msemaji wa UNHCR, Geneva.

(Sauti ya Fatoumata)

Katika hatua nyingine, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema siku chache zijazo litaanza mgao wa chakula kwa njia ya anga Sudan Kusini.