Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyakula vya kusindika kutoka nje ya nchi vyatishia afya za wakazi wa Pasifiki: FAO

Vyakula vya kusindika kutoka nje ya nchi vyatishia afya za wakazi wa Pasifiki: FAO

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limeonya kitendo cha kuendelea kuongezeka kwa maduka ya rejarejan kwenye nchi za visiwa vya Pasifiki yanayouza vyakula kutoka nchi za nje ambavyo vimesindikwa.

Hayo yamo katika mada iliyowasilishwa na FAO kwenye mkutano wa 32 wa ukanda wa Asia na Pacifiki unaofanyika huko Mongolia ambapo imesema vyakula hivyo licha ya kusababisha kutoweka madukani kwa vyakula vinavyozalishwa nchini humo, bali pia huathiri afya za walaji.

Hata vivyo FAO imesema ili kuhamasisha matumizi ya vyakula vilivyolimwa nchini humo na kupunguza uagizaji wa vyakula kutoka nje ya nchi, kunahitajika sera madhubuti zitakazochochea ongezeko la ulaji wa vyakula vya nyumbani kwa kukuza soko la ndani.

FAO inasema sanjari na kukuza soko pia itasaidia kupunguza viwango vya vifo na magonjwa vinavyotokana na ulaji wa mlo usio sahihi mathalani ulaji wa vyakula vilivyosindikwa.

Kwa sasa wavuvi kwenye nchi za Pasifiki hawawezi kukabiliana na ushindani wa vyakula kutoka nje ya nchi vilivyofungashwa kisasa na wengi wao wameamua kutelekeza kazi hiyo na kukimbilia mijini kusaka fursa mpya.

FAO inasema mlo katika kaya hizo ambao zamani ulisheheni vyakula vilivyolimwa au kuvuliwa nchini humo sasa umebadilika na kujumuisha vyakula vilivyosindikwa vilivyosheheni wanga, sukari, chumvi na mafuta ya viwandani ambavyo vyote vinatajwa kuhatarisha afya ya binadamu.