Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wimbi la wakimbizi kutoka Syria lalazimu Jordan kujenga kambi mpya

Wimbi la wakimbizi kutoka Syria lalazimu Jordan kujenga kambi mpya

Jordan itafungua kambi ya tatu kwa ajili ya kuhifadhi wakimbizi kutoka Syria ambao wanaendelea kumiminika nchini humo kila uchao kutokana na mapigano yanayoendelea nchini mwao. Hatua hiyo inakuja wakati shirka la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR likisema idadi ya wakimbizi wanaoingia Jordan kila siku kutoka Syria imeongezeka kwa asilimia hamsini na kufikia wastani wa wakimizi 600. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Kambi hiyo itakayofunguliwa eneo la Azraq takribani kilometa 100 mashariki mwa mji mkuu Amman, itahifadhi wakimbizi Laki Moja na Elfu Thelathini.

UNHCR imekaribisha mpango huo ikisema itasaidia kupunguza mlundikano kwenye kambi ya Za’atari ambayo ndiyo kambi kuu kwa wakimbizi hao wa Syria.

Kwa sasa kambi ya Za’atari inahifadhi wakimbizi wapatao Laki Moja kutoka Syria ambapo UNHCR inasema kiwango hicho ni kikubwa kupindukia.

Adrian Edwards ni msemaji wa UNHCR.

(Sauti ya Adrian)

Hadi leo zaidi ya makazi 2,500 yamekamilika, na hayo ni makazi thabiti siyo mahema! Makazi hayo kwa kuanzia yanaweza kuhifadhi wakimbizi 13,000. Tayari barabara zimejengwa, huduma za kujisafi kwa watu 30,000 , halikadhalika mfumo wa kusambaza maji umeshawekwa. Shule mbili, maeneo ya kuchezea watoto na vijana barubaru nayo pia yamekamilika pamoja na kituo cha afya. Kambi hiyo ikishafunguliwa itapokea wakimbizi wapya kutoka Syria, na tayari wakimbizi walioko nchini Jordan wanasubiri kwa hamu kuungana na wanafamilia watakaowasili.”

Kwa sasa Jordan inahifadhi takribani wakimbizi 585,000 kutoka Syria ambapo asilimia 80 kati yao wanaishi maeneo ya mijini nchini kote.