Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la kuzama kwa boti ghuba ya Aden lasikitisha UNHCR

Janga la kuzama kwa boti ghuba ya Aden lasikitisha UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeeleza masikitiko yake juu ya tukio jipya la kuzama kwa boti kwenye ghuba ya Aden mwishoni mwa wiki na kusababisha abiria 44 kutojulikana waliko hadi sasa, huku wengine 33 wakiwa wameokolewa.

Boti hiyo ilikuwa imebeba watu 77 wakiwemo wanawake, wanaume na watoto ambapo inaelezwa kuwa iliondoka bandari ya Bossasso huko Puntland kaskazini mwa pwani ya Somalia mapema Ijumaa ya tarehe Saba Machi.

Habari zinasema boti hiyo ilikumbwa na dhoruba kali kwenye pwani ya yemen na kwa mujibu wa mmoja wa manusura, boti hiyo ilijaa maji na kuzama.

Janga la kuzama kwa boti hiyo inaweka bayana mwelekeo wa wahamiaji na wakimbizi wanaosaka maisha bora kwingineko na UNHCR imezisihi serikali kwenye ukanda huo kuchukua hatua zinazoweza kusaidia kubaini watu wenye mahitaji ya kusaka hifadhi miongoni mwa hao wanaojitosa kusaka maisha bora kwa kusafiri kwa njia ya bahari.