Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia wabeba mzigo wa ghasia zinazoendelea Darfur Kusini: Pillay

Raia wabeba mzigo wa ghasia zinazoendelea Darfur Kusini: Pillay

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Navi Pillay ameeleza masikitiko yake kutokana na vile raia wanaendelea kukumbwa na madhila kutokana na mapigano yanayoendelea jimbo la Darfur Kusini nchini Sudan.

Amenukuu watu walioshuhudia matukio hayo wakisema kuwa vikundi vilivyojihami vinatumia nguvu kupita kiasi dhidi raia wasio na hatia.

Mathalani tangu mwezi Februari vijiji 45 kwenye eneo la Nyala, kusini mwa jimbo hilo vimeshambuliwa na licha ya kwamba si rahisi kukadiria raia waliouawa, yasemekana raia wapatao Elfu Hamsini wamepoteza makazi yao, makazi yao kuchomwa moto na mali kuporwa. Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Ravina)

“Kitengo cha haki za binadamu cha UNAMID, ambao ni ujumbe wa Umoja wa Mataifa hadi sasa umehesabu maiti tisini na watano ya raia na tathmini inaendelea.”

Kamishna wa haki za binadamu amesihi mamlaka husika kulinda raia na kuwawajibisha wale wote wanaohusika na uhalifu huo mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu za kimataifa.