WHO yatoa mwongozo wa huduma za kuzuia mimba

6 Machi 2014

Katika kuelekea siku ya wanawake duniani Machi 8, Shirika la afya duniani WHO limezindua muongozo mpya wa kusaidia nchi kuhakikisha haki za bindadamu zinaheshimiwa wakati wa kutoa huduma za afya ya uzazi kwa wasichana, wanawake na wapenzi kwa kuwapa taarifa zinazohitajika ili kuepukana na mimba zisizotakikana.

Alice Kariuki na taarifa kamili

TAARIFA YA ALICE

Takriban wasichana na wanawake milioni 222 ambao hawataki kushika mimba au wanaotaka kuchelewesha kushika mimba hawatumii mbinu zozote za kupanga uzazi. WHO imesema upatikanaji wa huduma ya kupanga uzazi kutasaidia katika kuweka mipango bora na kuimarisha afya.

Muongozo huo unapendekeza kwamba huduma hii iwe wazi kwa wanaoihitaji huku wakipatiwa taarifa zinazohitajika.

Dkt. Flavia Bustereo amabaye ni Mkurugenzi msaidizi wa Familia, wanawake na afya ya watoto katika WHO, anasema kwamba ukosefu wa huduma ya upangaji uzazi katika nchi zinazoendelea husababisha wanawake sita kati ya kumi kushika mimba zisizopangwa.

Ameongeza kuwa uwepo na upatikanaji wa huduma hii ni muhimu katika kuhakikisha haki za na wanawake na vile vile watoto zinazingatiwa.

Katika nchi za kipato cha chini, matatizo yatokanayo na uja uzito na uzazi ni miongoni mwa sababu kubwa ya vifo vya wanawake walio kati ya umri wa miaka 15-19. Pia wengi wa watu wasioweza kupata huduma hii ni vijana, maskini na wanaoishi vijijini na makazi duni mijini.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud