Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaonya kuibuka upya kwa mapigano kunazorotesha zaidi hali ya kibinadamu Sudani Kusini

UNICEF yaonya kuibuka upya kwa mapigano kunazorotesha zaidi hali ya kibinadamu Sudani Kusini

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaonya kuwa kuibuka upya mapigano nchini Sudani Kusini kutasababisha maelfu zaidi kukosa makazi ambapo hadi sasa takribani watu laki tisa nusu yao wakiwa watoto wamepoteza makazi yao.

Katika taarifa yake UNICEF inasema licha ya dalili ya makubaliano yakusitisha mapigano mwishoni mwa mwezi January mapigano baina ya serikali na upinzani yameongezeka katika siku za hivi karibuni. Kufuatia mapigano makali na taarifa za vifo vya watu katika makanisa na misikiti kaskazini mwa mji wa Malakal mwezi February shirika hilo la kuhudumia watoto linasema mapigano yamesambaa zaidi kaskazini mwa jimbo liitwalo Upper Nile na sasa kuna hofu kuwa takribani watu 30,000 wanaweza kukimbia makazi yao.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kuna mamia kwa maelfu ya wanawake na watoto pamoja na wanaume ambao hawapati maji ya kunywa, huduma za kujisafi, mlo na maji ya kuoga na kuongeza kuwa watoto wako katika mazingira hatarishi zaidi kutokana na milipuko wa magonjwa na ukosefu wa chakula

Hata hivyo pamoja na hali hiyo UNICEF inasongesha juhudi za kuwafikia wale waliopoteza makazi katika sehemu mbalimbali nchini Sudani Kusini wakiwamo watoto ambao wametenegan na familia zao na kutoa msaada wa kisaikolojia pale wanapolaimika kufanya hivyo.