Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya watoto Syria yalaaniwa

Mashambulizi dhidi ya watoto Syria yalaaniwa

Watoto wasio na hatia wamesalia kuwa wahanga wa vita nchini Syria ambapo katika shambulio la hivi karibuni zaidi mjini Homs watu zaidi ya 30 wamekufa na wengi kujeruhiwa wengi wao wakiwa watoto amesema mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kaika maeneo ya vita , Leila Zerrougui.

Bi Leila amesema katika taarifa yake kuwa watekelezaji wa shambulio hilo waliwalenga watoto wa shuleni na kusababisha kiwango kikubwa cha majeruhi.

Amesema mashambulizi shuleni na hospitalini yamekuwa ni hulka katika mgogoro wa Syria na hivyo kuangamiza haki za elimu na afya kwa mamilioni ya watoto ambapo tangu mwak 2011 zaidi ya watoto milioni  tatu wameacha shule huku maelfu ya shule zimeharibiwa au kutumiwa na vikundi vya kijeshi.

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto kayika maeneo ya vita amesema kulenga shule na watoto ni uhalifu wa kupindukia dhidi ya sheria za kibinadamu za kimataifa na kuongeza kuwa hata nyakati za vita shule na hospitali lazima zisalie salama kwa kujifunzia na kupata huduma za afya. Pia ametaka pande kinzani kusitisha mashambulizi na watekelezaji wafikishwe kwenye mkono wa sheria.