Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Angelina Jolie ashuhudia madhila ya wakimbizi wa Syria huko Lebanon

Angelina Jolie ashuhudia madhila ya wakimbizi wa Syria huko Lebanon

Mjumbe maalum wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Angelina Jolie amezuru kambi za wakimbizi wa Syria nchini Lebanon na kushuhudia madhila yanayowakumba ikiwemo kukosa huduma za msingi ikiwemo afya na elimu.

Akiwa ziarani humo kwa siku tatu muigizaji huyo mashuhuru wa Hollywood, amekutana na watoto yatima kwenye jimbo la Bekaa na kusema kuwa ni wadogo mno kubeba jukumu la kujitunza wao wenyewe bila familia zao.

Mathalani alikutana na mtoto mmoja wa kiume ambaye alimweleza matamanio yake ya kuwa daktari pindi atakapokuwa mtu mzima lakini wadogo zake wakaanza kumcheka ya kwamba haelewi kilichomkumba kwani anawezaje kuwa daktari ndani ya hema tupu.

Bi. Jolie ameelezea mchango wa dhati wa Lebanon katika kuhifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa Syria ambapo idadi yao inakaribia Milioni Moja. Amekuwa na mazungumzo na viongozi wa Lebanon kuhusu athari za wakimbizi na kuwashukuru kwa mchango wao wa ku wahifadhi huku akitaka jamii ya kimataifa kuongeza usaidizi.

Hii ni ziara ya tatu ya Angelina Jolie kwa niaba ya UNHCR nchini Lebanon mara ya mwisho alikuwemo nchini humo mwezi Septemba mwaka 2012.