Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa CAR ni mkubwa wa aina yake:Ban

Mgogoro wa CAR ni mkubwa wa aina yake:Ban

Mgogoro unaoendelea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ni mkubwa wa aina yake unaohitaji hatua ya haraka ya jumuiya ya kimataifa, amesema katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Katika taarifa yake kwenye baraza la haki za binadamu kwenye ufunguzi wa kikao maalumu kuhusu halki nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ban ametoa wito wa kumaliza mzunguko wa machafuko na kulipiza kisasi.

Ameonya kwamba endapo ghasia azitodhibitiwa basi huenda zikasababisha mauaji zaidi. Taarifa hiyo ya Ban imesomwa na mkurugenzi mkuu wa ofisi ya Umoja wa mataifa Geneva Michael Moller.

(SAUTI YA MICHAEL MOLLER)

"Mivutano ya kidini haiwahi kuwa sehemu ya CAR huko nyumba na ni lazima isiwe sehemu ya nchi hiyo siku za usoni. Pia ninatoa wito kwa wote kutoa kipaumbele kwa maridhiano ya kitaifa na amani ya kudumu. Hii itahitaji kuanzishwa tena kwa uongozi imara na mfumo wa sheria , ambavyo vitazingatia utawala wa sheria na kulinda haki za binadamu. Ni lazima tuunge mkono serikali ya mpito katika changamoto zinazoikabili. Hakutakuwa na maridhiano bila uwajibikaji. Kwa mujibu wa azimio la baraza la usalama namba 2127, Umoja wa Mataifa unaanzisha tume ya kimataifa ya uchunguzi kunukuu ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu. Tume hii muhimu pamoja na mtaalamu wa baraza la haki za binadamu watashirikiana kwa karibu katika wajibu wao wa kupambana na ukwepaji wa sheria na kulinda haki za binadamu Jamhuri ya Afrika ya Kati.”

Katibu Mkuu ameitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua ahatua ya pamoja na kwa mshikamano, kulinda watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuwasaidia kuondoka katika hali ya ufukara na kukata tama na kuelekea kwenye njia ya matumaini.