Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia yapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidia Syria: Mkuu wa OCHA

Dunia yapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidia Syria: Mkuu wa OCHA

Hali ya kibinadamu kwa zaidi ya raia Milioni Tisa Nukta Tatu wa Syria ni mbaya sana na hivyo dunia yapaswa kuchukua hatua zaidi, amesema Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa masuala ya kibinadamu Valerie Amos wakati alipohitimisha ziara yake huko Damascus, Syria, Jumapili. Akizungumza na wadau wa masuala ya kibinadamu na wale wa serikali mjini humo, amesema kauli yake inazingatia hali inayokumba wasyria hususan wale walionasa kwenye maeneo yenye mapigano kati ya majeshi ya serikali na wapinzani na hawajaweza kupata misaada kwa miezi kadhaa sasa. Bi. Amos ambaye ni mkuu pia wa shirika la usaidizi wa kibinadamu la Umoja wa Mataifa, OCHA amesema hofu yake zaidi ni ripoti ya kwamba watu hao wanakabiliwa na njaa. Amesema wakati jamii ya kimataifa inajiandaa kwa mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usaidizi wa kibinadamu nchini Syria, ametaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua zaidi mwaka huu wa 2014 ili misaada iweze kuwafikia wale wanaohitaji zaidi. Ameweka bayana kuwa wasyria wengi wanaishi kwenye majengo yaliyotelekezwa, au kwenye makazi ya kuhamahama bila huduma za msingi kama vile maji safi, afya na hata maliwato. Mkutano wa usaidizi kwa Syria utafanyika Kuwait tarehe 15 mwezi huu ilhali mazungumzo ya amani yatafanyika tarehe 22 huko Motreaux, Uswisi.