Shehena ya kwanza ya vifaa vihusikanavyo na silaha za kemikali Syria yang’oa nanga Lattakia

7 Januari 2014

Hatimaye shehena ya kwanza ya vifaa vinavyohusika na silaha za kemikali nchini Syria imesafirishwa kutoka nchini humo kupitia bandari ya Lattakia. Taarifa hizo zimethibitishwa na  mratibu wa Jopo la pamoja la Umoja wa Mataifa na shirika la kimataifa la kupinga silaha za kemikali OPCW, Sigrid Kaag. Katika taarifa yake Bi. Kaag  amesema vifaa hivyo vilisafirishwa kutoka maeneo mawili muhimu hadi bandari hiyo na baadaye kupakiwa kwenye meli ya Denmark. Meli hiyo tayari imeondoka Lattakia na inasindikizwa na meli za wanamaji kutoka Denmark, Norway na serikali ya Syria. Hatua ya leo ni utekelezaji wa mpango wa kusafirisha vifaa hivyo kwenda nchi ya kigeni. Hata hivyo meli hiyo itabakia eneo la kimataifa baharini ikisubiri nyongeza zaidi ya vifaa hivyo. Taarifa hiyo inazitajaChina, na Urusi kutoa usaidizi wa ulinzi kwa meli hiyo baharini. Bi. Kaag amesema kinachofanyika sasa ni kuendelea kuratibu nchi wanachama, hususanSyriayenyewe kuchangisha rasilimali na kuchukua hatua muhimu ili kukamilisha utokomezaji wa mpango wa silaha za kemikali.