Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNIDO ina dhima muhimu kuelekea uzalishaji viwandani ulio rafiki kwa mazingira: Ban

UNIDO ina dhima muhimu kuelekea uzalishaji viwandani ulio rafiki kwa mazingira: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amefungua mkutano Mkuu wa 15 wa Shirika la maendeleo ya viwanda la Umoja wa Mataifa , UNIDO huko Lima, Peru akiangazia umuhimu wa taasisi hiyo katika kuwezesha dunia kufikia maendeleo endelevu hata baada ya mwaka 2015.

Bwana Ban amesema sasa kuna kasi ya kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia ifikapo mwaka 2015 lakini kuna changamoto kubwa ya suala la ajira na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema miaka 40 iliyopita mji wa Lima uliweka historia ya kupitisha azimio la kuwezesha nchi changa kunufaika na uzalishaji wa viwandani na leo tena mji huo utaibuka na historia ya kuweka fursa sawia ya maendeleo endelevu ya viwandani na jumuishi. Bwana Ban amesema katika kutekeleza nyaraka hiyo na hata kufikia malengo endelevu UNIDO ina dhima muhimu.

(Sauti ya Ban)

“Dunia haiwezi kufikia malengo ya maendeleo bila ubia na viwnda vinayochochea ukuaji na ajira. Hatuwezi kutokomeza umaskini bila viwanda vinavyoendeleza ubunifu na uenezaji wa teknolojia. Maendeleo ya viwanda yanaweza pia kuwa mwezeshaji mkuu na injini ya maendeleo ya kijamii kwa kuweka fursa za ajira kwa wanawake na vijana. Pili UNIDO inaweza kuweka kasi ya mazingira endelevu, hiyo inanipeleka kwenye eneo la tatu kuwa UNIDO inaweza kuchangia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.”

Bwana Ban amesema ameweka matumaini yake kwa UNIDO katika kutoa ushauri wa kitaalamu na kusaidia mabadiliko ya kasi ya sekta ya viwanda duniani ili kuwa na mifumo na miundo ya uzalishaji ya kibiashara isiyo na madhara kwa mazingira.