Baraza Kuu lajadili ufanyiaji Baraza la Usalama Marekebisho

7 Novemba 2013

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limekutana kujadili suala la kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama, ambalo limekuwa likizua utata katika mijadala mingi ya Umoja wa Mataifa. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Suala la kutaka kufanyia marekebisho Baraza la Usalama limekuwa likiibuka katika vikao vingi vya mijadala mikuu ya Baraza Kuu. Leo basi, katika mjadala mwingine, suala la usawa katika uwakilishi kwenye Baraza la Usalama na kutaka idadi ya wawakilishi wake iongezwe, limepewa kipaumbele. Akiufungua mjadala wa leo, rais wa Baraza Kuu, John William Ashe, amesema suala hilo linamhusu kila mmoja, na kupiga hatua katika kufanyia marekebisho Baraza la Usalama, ni lengo la wote.

“Wengi wenu mtakumbuka kuwa, nilipochaguliwa kuwa rais wa Baraza Kuu, nililisitiza haja ya kuanzisha tena na kuendeleza suala la kufanyia marekebisho Baraza la Usalama, na nilisisitiza kuwa nitalipa kipaumbele. Huku utashi huu ukisalia thabiti, siwezi kupuuza changamoto zilizopo.”

Akiongea kwa niaba ya nchi za bara la Afrika, Mwakilishi wa Kudumu wa Siera Leone, Vandi Chidi Minah amesema:

“Ningependa kusisitiza utashi wa nchi wanachama wa Muungano wa Afrika kwa suala hili muhimu. Bado tunaamnini kuwa kuna haja ya marekebisho ya kina kwa mfumo mzima wa Uoja wa Mataifa, ili uendeleze misingi ya Mkataba Mkuu kwa ulimwengu wenye haki, usawa na uwakilishi wa kila ukanda, na kuhakikisha kuwa Baraza la Usalama ni jumuishi, linawajibika, ni wazi, linafikika na pia linatimiza majukumu yake.”

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter