Ombi la ufadhili wa dharura latolewa wakati Mali ikiachwa bila wafadhili

22 Oktoba 2013

Watu wanaoishi katika eneo la Sahel barani Afrika ni miongoni mwa watu walio hatarini zaidi duniani, na matatizo yanazidi kuibuka mara kwa mara, imesema Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, OCHA. OCHA imesema ukosefu wa ufadhili kutoka kwa jamii ya kimataifa ni mojawapo wa sababu kuu ya misaada kutowafikia watu wanaoihitaji kwa dharura.

Msaidizi wa Katibu Mkuu ambaye pia ni Mratibu wa OCHA kwa ukanda wa Sahel, Robert Piper amesemataifa la Mali linahitaji kusaidiwa kwa dharura ili watu waweze kufikishiwa huduma za kimsingi kama vile elimu, afya, umeme na maji, ambavyo ni haba kupatikana hususan katika eneo la kaskazini mwa nchi.

Amesema mikakati mipya inahitajika ili watoaji huduma za dharura waweze kukabiliana na matatizo ya mara ka mara Mali na ukanda wa Sahel.

 “Mali huenda ikawa ndiyo nchi ilopata ufadhili mdogo zaidi katika ukanda mzima. Ina mahitaji ya dharura zaidi ya kibinadamu- ukizingatia machungu wanayopitia, utapiamlo, usalama wa chakula, hasa maeneo ya kaskazini mwa nchi. Ilipata ahadi kubwa zaidi kuwahi kutolewa wakati wa mkutano wa wafadhili mjini Brussels mwezi Mei, wakati wafadhili waliahidi kutoa dola bilioni moja zaidi ya fedha zilizoombwa. Licha ya hayo, ombi la ufadhili kwa ajili ya Mali limepata asilimia 40 tu, ambalo ndio ufadhili mdogo zaidi hata kuunshinda ule wa Gambia”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter