Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN-Women kuelekea ukomo wa Malengo ya milenia kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike

UN-Women kuelekea ukomo wa Malengo ya milenia kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa shirika la umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN-Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema wakati ulimwengu ukijitihadi kufikia malengo ya milenia kabla ya ukomo wake mwakani, shirika lake litatumia fursa hiyo kuimarisha huduma muhimu kwa mwanamke ili kufikia lengo la ukombozi wa kundihilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani siku ya Alhamisi, Bi. Mlambo-Ngcuka amesema fursa ya kufikia malengo hayo ni fursa pia ya kuchochea upatiaji mwanamke na mtoto wa kike elimu bora, afya bora ya uzazi na fursa stahili za kiuchumi ili waweze kujikomboa.

(Sauti ya Phumzile)

Kati ya sasa na 2015 nimeazimia kufanya kazi kwa kina na watoa huduma, taasisi, mashirika kuhakikisha kile tunachoweza kufanya sasa kinafanikiwa. Hasa hasa nitaje elimu kwa mtoto wa kike ambapo sasa kuna shinikizo kubwa kiasi kwamba katika kipindi hiki sisi UN-women tunaweza pia kusaidia watoto wa kike kupata elimu na kupunguza idadi ya watoto hasa  wa kike wanaotoroka shule, hili ni jambo nitakalopatia kipaumbele.”

Mkurugenzi mtendaji huyo mpya wa UN-Women akaulizwa kuwa ubaguzi wa wanawake ambao umejikita siyo tu katika nchi maskini bali pia zile zilizoendelea, sasa atafanyaje kushughulikia suala hilo.?

(Sauti ya Phumzile)

“Mtazamo wa kiuharakati kwa suala hili ni muhimu. Kwa sababu iwapo serikali zimekubali kushughulikia suala hilo na hazifanyi  hivyo, ni wajibu wa wananchi kwa msaasda wa Umoja wa Mataifa kuwajibisha serikali. Ambako kuna ubaguzi kwenye sekta binafsi, sisi tunahamasisha soko lao, na wanawake ni soko kubwa kwenye uchumi, kwa hiyo watazipatia changamoto tabia hizo za kibaguzi.”