Naibu Katibu Mkuu wa UM asisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya usafi:

3 Septemba 2013

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesisitiza umuhimu wa kushughulikia masuala ya usafi na kujisaidia hadharani. Bwana Eliasson ameyasema hayo mjini Stockholm, Sweden ambako mamia ya wajumbe kutoka kote duniani wanakutana katika wiki ya maji duniani. Akitoa ujumbe maalumu kwa wiki hii chini ya kauli mbiu “kujenga ushirikiano kwa ajili ya usafi na maji kwa wote” amekumbushia tangazo la mwaka jana kwamba dunia imefikia lengo la kuwa na vyanzo bora vya maji. Hata hivyo ameongeza kuwa ukosefu wa usafi unaathiri ubora wa maji katika nchi masikini.

Amesema zaidi ya watu bilioni 2.5 duniani hawana hali ya usafi inayostahiki na bilioni moja kati yao wanajisaidia hadharani. Wiki ya maji inaadhimishwa rasmi mjini Stockholm kuanzia tarehe 1 hadi 6 Septemba. Mamia ya wawakilishi wa serikali, biashara , wanazuoni na jumuiya za kijamii wanafanya warsha , semina na mikutano mingine kuhusu maji na usafi kwa wote.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter