Tunafuatilia mchakato wa kufikia malengo ya haki za binadamu:Pillay

5 Agosti 2013

Wakati kilele cha malengo ya maendeleo ya milenia kikijongea Umoja wa Mataifa na washirika wake wanajadili mkakati ambao utafanikisha nia yao.Mkakati huo ni ajenda baada ya 2015 ambayo pia bado ina lengo la kutokomeza umasikini uliokithiri na kuweka suala la maendeleo endelevu kuwa kitovu cha mabadiliko na wana lengo la kufikia azima hiyo ifikapo 2030.

Mbali ya mipango ya baada ya 2015 kikubwa kimekuwa ni kutathimini njia zilizotumika kupima hatua zilizofikiwa katika malengo manane ya maendeleo ya milenia yaliyokubaliwa mwaka 2000.

Ofisi ya haki za binadamu imekuwa ikifanya kazi na kitengo maalumu kilichoanzishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kupitia takwimu zilizokuwepo  na kuzifasiri, na kasha kuandaa utaratibu maalumu utakaotumika baada ya mwaka 2015.

Kamishna mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ambayo imeandaliwa na kitengo maalumu ikijumuisha mchango kutoka vitengo zaidi ya 60 vya Umoja wa mataifa amesema malengo ya milenia na viashiria vyake sio wakati wote yalizingatia wajibu wa kutimiza mikataba ya haki za binadamu katika mataifa mbalimbali, na kwingineko watu wamelifumbia macho suala la ubaguzi.

Ripoti hiyo imehitimishwa kwa kusema juhudi zaidi zinahitajika kuzisaidia nchi kuanzisha huduma ya kitaifa ya takwimu.