Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakhbali wa vijana wajadiliwa Umoja wa Mataifa

Mustakhbali wa vijana wajadiliwa Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa na ulimwengu mzima unajiandaa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana mnamo Agosti 12, na leo mdahalo maalum umefanyika kuhusu mikakati ya Umoja wa Mataifa inayohusiana na masuala ya vijana, kama sehemu ya maadhimisho ya siku hiyo. Joshua Mmali amekuwa akiufuatilia.

(TAARIFA YA JOSHUA)

Mdahalo wa leo umewajumuisha vijana kutoka nchi mbalimbali zilizowakilisha kila pembe ya dunia, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon na viongozi wengine wa ngazi ya juu katika Umoja wa Mataifa, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Idadi ya Watu, UNFPA, Babatunde Osotimehin. Mdahalo huo umesimamiwa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa masuala ya vijana, Ahmad Alhendawi,

 SAUTI YA ALHENDAWI

 Ujumbe wangu kwa vijana ni kwama Umoja wa Mataifa unajikita kwa masuala ya vijana, na tunataka kufanya kazi nanyi. Tutazindua mikakati mbali mbali na njia za kuwajumuisha vijana katika Umoja wa Mataifa, yakiwemo makongamano ya kikanda, kwa ushirikiano na Baraza la Uchumi na Jamii. Ofisi zetu za kitaifa pia zitaanzisha bodi za ushauri wa vijana kwa ngazi za kitaifa, na tunataka kusikia mawazo ya vijana. Tunawafikia kupitia vyombo vya habari vya kijamii, kupitia tovuti, na mikakati mbali mbali, na tunatakiwa kufanya kazi pamoja.

Mdahalo umeanza kwa hotuba fupi ya Katibu Mkuu, Ban Ki-Moon, ambaye amesema amewaweka vijana katika ajenda zake tano za hatua za kipaumbele

 SAUTI YA BAN

Kufanya kazi na vijana kwa ajili yao ni jambo la kipaumbele kwa Umoja wa Mataifa. Nusu ya idadi ya watu wote duniani ni chini ya miaka 25. Mnataka nafasi zaidi na za ajira bora, elimu nzuri, upatikanaji wa huduma za afya za gharama nafuu, serikali zenye uwazi na zinazowajibika zaidi, na juhudi zaidi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Mna mambo mengi, na mawazo mbalimbali ambayo tungependa kusikia.

Baadaye Bwana Ban ameulizwa maswali na vijana kutoka Nigeria, India, Ubeljiji, Brazil na Lebanon, pamoja na wale ambao wamekutana kwenye ukumbi wa Baraza Kuu hapa mjini New York.