Unyonyeshaji maziwa ya mama bado wakumbwa na kikwazo: WHO

30 Julai 2013

Ni nchi 37 tu duniani sawa na asilimia 19 tu ambazo zimepitisha sheria zinazoelekeza mapendekezo juu ya matumizi ya maziwa ya kopo kwa watoto wachanga kama mbadala wa maziwa ya mama, hiyo ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO katika ripoti yake kuelekea kuanza kwa wiki ya unyonyeshaji duniani Agosti Mosi.

Mtaalamu wa unyonyeshaji maziwa ya mama kutoka WHO Dkt. Carmen Casanovas amesema kila mama ana uwezo wa kunyonyesha na iwapo mama atapata taarifa sahihi juu ya unyonyeshaji atafanya hivyo. Hata hivyo amesema mara nyingi hulaghaiwa na kukatishwa tamaa na kuaminishwa kwamba mtoto anakua vizuri iwapo ataanzishwa mapema maziwa ya kopo.

WHO inasema maziwa ya mama ni chanzo kizuri cha lishe bora kwa watoto kuanzia wachanga na ni hakikisho bora la uhai na makuzi ya mtoto. Linasema watu walionyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi Sita wana nafasi ndogo sana ya kuwa matipwatipwa, kupata ugonjwa wa kisukari na wana uelewa mkubwa wa mambo lakini dunia nzima ni asilimia 38 tu ya watoto ambao wamenyonya maziwa ya mama pekee kwa kipindi hicho.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter