Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuendelea kukariri uhalifu unaoendelea Syria bila vitendo hakutoshi: Pinheiro

Kuendelea kukariri uhalifu unaoendelea Syria bila vitendo hakutoshi: Pinheiro

pinhMkuu wa Tume huru ya kimataifa ya kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Syria, Paulo Pinheiro, ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa kuendelea kukariri vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Syria bila kufanya lolote hakutoshi, huku akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua. Joshua Mmali anayo taarifa zaidi

Akiongea katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambalo leo limekutana kusikiliza ripoti ya uchunguzi katika madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Syria, Bwana Paulo Sergio Pinheiro amesema taifa la Syria linaendelea kuporomoka, huku machafuko yakizidi kutokota.

Bwana Pinheiro amesema uhalifu wa kushangaza unaendelea kutendeka dhidi ya raia, na huku wale wanaoutekeleza ukiukwaji huo wa haki za binadamu wakiendelea tu bila kuogopa kuchukuliwa hatua yoyote dhidi yao.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu amesema, kutokuwepo hatua yoyote kutoka kwa jamii ya kimataifa kumechochea kunawiri kwa desturi ya uhalifu bila kuogopa kuchukuliwa hatua za kisheria. Amesema kukariri tu uhalifu unaotendeka na kuutaja kama wa kushangaza bila kuchukuwa hatua hakutoshi.

Ni lazima kuwepo usitishwaji mapigano ili misaada ya kibinadamu ichukuliwe kwa urahisi kote nchini, na kutoa fursa kwa hatua za kwanza za mazungumzo kufanyika. Ni wakati wa jamii ya kimataifa kuchukua hatua thabiti. Hakuna uamuzi rahisi. Lakini kukwepa kuchukua msimamo ni kuendelea kutizama kuendelea kwa mzozo huu na ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu. Mna wajibu, na hamna budi kufanya mnalohitajika kufanya kukomesha vita hivi.

Tangu ilipoundwa mwaka 2011, tume hiyo ya uchunguzi imetoa ripoti kumi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Syria, na inatarajiwa kuwasilisha ripoti nyingine kwenye Baraza la Haki za Binadamu mnamo Septemba 16, mjini Geneva.