Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo maalum lamulika utumiaji wa mamluki katika shughuli za UM

Jopo maalum lamulika utumiaji wa mamluki katika shughuli za UM

Utumiaji wa kampuni za kibinafsi za kutoa huduma za kiusalama katika Umoja wa Mataifa umemulikwa leo katika mkutano wa jopo maalum lililowekwa na Baraza la Haki za Binadamu kufuatilia shughuli za mamluki katika huduma za Umoja wa Mataifa. Joshua Mmali amefuatilia mdahalo wa jopo hilo:

TAARIFA YA JOSHUA MMALI

Umoja wa Mataifa hivi sasa unatumia kampuni za ulinzi za kibinafsi katika shughuli mbalimbali za kiusalama katika maeneo mengi kote duniani. Kampuni hizo hutoa huduma kwa Umoja wa Mataifa katika usafirishaji wa vifaa na misaada, kutathmini hatari za kiusalama, kutoa mafunzo na ushauri wa kiusalama, na wakati mwingine, walinzi wenye silaha.

Wahusika katika jopo hilo wamesema hili ni suala ambalo linaathiri kila sehemu ya jamii ya kimataifa, hususan wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, nchi wanachama, mashirika ya umma na kampuni zenyewe. Anton Katz kutoka Afrika Kusini ni mwenyekiti wa sasa wa jopo hilo

Jopo hili linaamini kuwa Umoja wa Mataifa una nafasi na wajibu wa kuhakikisha kwamba viwango vya kampuni za kibinafsi za ulinzi vinaenda sambamba na viwango vya kimataifa vya kanuni za haki za binadamu. Umoja wa Mataifa unatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na nchi wanachama na mashirika mengine ambayo hutumia kampuni kama hizo, kwa kuhakikisha viwango timamu na umakini wakati unapozishirikisha kampuni za kibinafsi katika huduma zake.

Mazungumzo ya leo yameangazia mwongozo wa idara ya usalama katika Umoja wa Mataifa kuhusu matumizi ya kampuni za ulinzi za kibinafsi, ambao ulichapishwa mnamo mwaka 2012 kama sehemu ya sera ya Umoja wa Mataifa kuhusu matmizi ya mamluki.