Sote tuna wajibu wa kutokomeza adhabu ya kifo: Ban

28 Juni 2013

Tuna wajibu wa kuzuia watu wasio na hatia kuwa wahanga wa ukiukwaji wa haki, hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliyotoa kwenye kikao cha ngazi ya juu mjini New York Marekani kuhusu utokomezaji wa adhabu ya kifo.Bwana Ban amesema njia ya kiungwana zaidi ni kuachana na adhabu hiyo ya kikatili ambapo amesifu nchi zilizo kwenye mjadala wa kitaifa wa kutokomeza adhabu hiyo kufuatia wito wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka 2007 wa kutaka dunia nzima kutokomeza kitendo hicho.

Katibu Mkuu ametaka nchi ambazo bado zinatekeleza adhabu hiyo kuachana nayo na zile ambazo zimeanza upya baada ya kusitisha kwa muda kufikiria uamuzi wao. Hata hivyo Bwana Ban akazungumzia wasiwasi wake ambao ataelezea kwa kina kwenye ripoti yake ijayo juu ya adhabu ya kifo.

“Ripoti yangu ijayo itaelezea hofu kubwa juu ya kwamba adhabu ya kifo hutendeka kisiri. Ukosefu wa takwimu za waliotekelezewa adhabu hiyo au walio katika orodha ya adhabu ya kifo ni kizingiti kikubwa cha mjadala wa kitaifa kuhusu adhabu ya kifo. Lakini ni mjadala ambao unapaswa kuendelea hadi dunia iwe huru dhidi ya kitendo hiki katili.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud