Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi yaahidi kuchochea utokomezaji ajira kwa watoto majumbani

Malawi yaahidi kuchochea utokomezaji ajira kwa watoto majumbani

Wakati dunia hii leo inaadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ajira kwa watoto, Rais Joyce Banda wa Malawi amezungumza katika mkutano wa 102 wa kimataifa wa shirika la kazi duniani, ILO na kusema nchi yake itachochea harakati za kupiga vita vitendo hivyo dhalimu kwa watoto vinavyowanyima haki zao za msingi ikiwemo kwenda shule. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

 

Hotuba  ya Rais Banda imeenda sambamba na siku ya kimataifa ya kutokomeza ajira kwa watoto hii leo ikimulika zaidi, ajira za majumbani. Rais Banda amewaeleza washiriki wa mkutano  huo mjiniGeneva, Uswisi ya kwamba yeye binafsi anasikitishwasanana ajira za watoto hususan kwenye nchi zinazoendelea ikiwemoMalawi, akitaja chanzo kuwa ni umaskini. Amesema familia maskini zisizo na ajira zenye hadhi zinajikuta watoto wao wakitumbukia kwenye ajira za utotoni. Amesema ukuaji wa uchumi waMalawikwa asilimia sita kati ya mwaka 2004 na 2009,  haukuweza kuepusha watoto na ajira kwa kuwa haukutoa fursa za ajira za kutosha. Na ndipo akatoa ahadi.

 

(SAUTI YA Rais BANDA)

“Naahidi kuendelea na harakati za kutokomeza ajira kwa watoto nchini Malawi, na pia kuimarisha mipango ya kutokomeza umaskini ambao ni chanzo kikuu cha tatizo hilo.Nategemea ILO kama shirika la kufanya nalo kazi kwenye suala hili.”

 ILO inasema zaidi ya watoto Milioni Kumi na Nusu wengine wakiwa hata na umri wa miaka mitano wanahusishwa na ajira za majumbani, na wengi wao ni watoto wa kike.