WFP na UNFPA zamulika lishe bora kwa wajawazito

7 Juni 2013

Shirikal la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP na lile la idadi ya watu duniani, UNFPA wanazindua ushirikiano mpya wa kuboresha lishe miongoni mwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha ili kuhakikisha kizazi kijacho cha watoto kinapata makuzi mazuri. Alice Kariuki anaripoti.(RIPOTI YA ALICE KARIUKI)

Mpango huu mpya unazinduliwa kabla ya kuandaliwa kwa mkutano kuhusu lishe mjiniLondon, Uingereza tarehe nane mwezi huu kujadili lishe kwa wanawake wakati wakiwa wajawazito na wanaponyonyesha.

Lengo ni kuzuia kuzaliwa watoto walio na uzito wa chini na wale wasiokua ambao wanakabiliwa na matatizo ya kiafya na kukumbwa na matatizo ya kufanikiwa kimasomo na kichumi.

Ushirikiano kati ya WFP na UNFPA unaunga mkono mipango 1000 inayolenga kuboresha lishe katika kipindi cha siku 1000 za kwanza kati ya wakati wa ujauzito hadi mtoto anapofikia umri wa miaka miwili.

Wakiwa na nafasi kubwa mashinani WFP na UNFPA wako katika hali nzuri ya kuwafikia wanawake wanapotembea zahanati kuwapa ushauri kuhusu afya ya uzazi na jinsi wanaweza kupata vyakula muhimu wakiwa na ujauzito.