Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na hazibagui: Ban

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na hazibagui: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza katika chuo cha taifa cha utafiti wa masuala ya anga huko Boulder,Coloradonchini Marekani na kusema kuwa ajenda kuhusu mabadiliko ya tabianchi sasa imechukua hatua kwa kuwa madhara yake hayaongopi na hayabagui na sasa yanagusa hadi hatma ya usalama na utulivu wa nchi.  Bwana Ban amewaeleza wasomi chuoni hapo ya kwamba tafiti za wanasayansi kuhusu anga zimedhihirisha kuwa kiwango cha joto duniani kinaongezeka na utoaji wa hewa chafuzi umezidi kiwango na madhara yake yanashuhudiwa. Ametaja madhara hayo kama vile vimbunga vya kupindukia, tufani na hata mioto ya porini ya mara kwa mara ambapo ametumia fursa hiyo kuwapongeza wanasayansi kwa msimamo wao wa kueleza ukweli na kuepuka kuyumbishwa na makundi kama vile wanasiasa au watu wasio na matumaini juu ya ukweli kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Bwana Ban amesema tafiti na takwimu za wanasayansi zinasaidia kutunga sera na kwamba yeye binafsi amelivalia njuga suala la kutafuta utashi wa kisiasa ili kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Kwa mantiki hiyo amesema anasubiri kwa hamu ripoti ya tathmini tano kuhusu mabadiliko  ya tabianchi itakayotolewa mwezi Septemba mwaka huu hukoStockholmSweden, ripoti ambaye amesema itatoa mwelekeo wa athari za mabadiliko ya tabianchi duniani. Akiwa Colorado, Bwana Ban anazungumza pia na wanafunzi wa chuo kikuu cha Denver.