TEKNOHAMA ichochee usalama barabarani: Ban

17 Mei 2013

Katika kilele cha siku ya jamii habari duniani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa ujumbe unaotaka maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, TEKNOHAMA yawe kichocheo cha kuimarisha usalama barabarani.Bwana Ban amesema msimamo huo unazingatia takwimu za hivi punde ya kwamba watu ajali za barabarani kila mwaka husababisha vifo vya watu zaidi ya Milioni Moja na Laki Tatu na wengine wengi kubaki na vilema vya maisha na hivyo kusababisha gharama kubwa kwa familia na nchi husika.

 Amesema mifumo ya kisasa ya usafiri na vifaa vya kufuatilia mienendo ya magari inaweza kupunguza misongamano na migongano hususan na waenda kwa miguu huku akiongeza kuwa vifaa vya mawasiliano visivyolazimu dereva kushikilia wakati anaendesha gari vinaweza kupunguza ajali.

 (SAUTI YA BAN)

 Maadhimisho hayo yamefanyika huku mkutano wa kimataifa wa jamii habari ukihitimishwa huko Geneva, Uswisi ambapo tuzo ya jamii habari duniani kwa mwaka huu wa 2013 imekwenda kwa watu watatu mashuhuri ambao ni Rais wa shirikisho la Uswisi Ueli Maurer, Volkmar Denner na Jean Todt kwa jinsi walivyojitoa kuhakikisha TEKNOHAMA inatumika kupunguza ajali za barabarani.