Ukiukwaji wa sheria Jamhuri ya Afrika ya Kati ukome: Pillay

16 Aprili 2013

Hali ya sintofahamu inazidi kukumba Jamhuri ya Afrika ya Kati huku idadi ya watu waliouawa tangu waasi wapindue serikali ikiongezeka na raia wakikimbilia nchi jirani.

Umoja wa Mataifa umetaka kukomeshwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamukamaanavyoarifu Assumpta Massoi.

 (ASSUMPTA PKG )

 Zaidi ya watu 119 wameuawa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu waasi wapindue serikali mwezi uliopita, taarifa hizo ni kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Inaelezwa kuwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vimeshamiri, mathalani mauaji, utekaji nyara, watu kuwekwa vizuizini na kuteswa, watoto kutumikishwa na hata ubakaji na watu kupotea katika mji mkuuBanguina maeneo mengine ya nchi hiyo. Kufuatia hali hiyo Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu Navi Pillay ametaka utawala wa kisheria kurejeshwa na wahusika wawajibishwe. Cécile Pouilly ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

 (SAUTI YA CECILY)

 “Makundi mbali mbali yameshutumiwa kujilimbikizia mali, kuna  uporaji wa mali binafsi na ya umma kutoka vituo vya afya , ofisi za misaada ya kibinadamu na mabohari.  Hali ya sasa ya ukosefu wa sheria haiwezi kuruhusiwa kuendelea. Wanaofanya ukatili wa kupindukia hususan viongozi wao wanapaswa kutambua kuwa kila mmoja anawaweza kuwajibishwa kivyake kutokana na uhalifu huo.”

 Katika hatua nyingine shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema idadi ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanaokimbilia nchi jirani inaongezeka. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina wakimbizi zaidi ya Elfu 30,Chadzaidi ya 6500 naCameroonzaidi ya Elfu Moja.