Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama za kimataifa za uhalifu zimedhihirisha hakuna aliye juu ya sheria: Ban

Mahakama za kimataifa za uhalifu zimedhihirisha hakuna aliye juu ya sheria: Ban

Marais wa mahakama za kimataifa za uhalifu wamekuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon huko The Hague Uholanzi ambapo Bwana Ban amesema kazi zilizofanywa na mahakama hizo kwa kipindi cha miongo miwili zimedhihirisha kuwa hakuna mtu yeyote yule aliye juu ya sheria.

Amesema uendeshaji wa kesi katika mahakama hizo ikiwemo ya ICC na zile maalum zinazohusika na iliyokuwa Yugoslavia, ya Sierra Leone, Lebanon na Rwanda umehakikisha uwajibikaji kwa wale wote waliofanya makosa dhidi ya kibinadamu na hivyo kuepusha vitendo hivyo kujirudia.

Bwana Ban amesisitiza umuhimu wa kusimamia haki katika mchakato wowote wa maridhiano na kusema kwamba harakati za kuzuia mauaji ya kimbari ni suala linalopatiwa kipaumbele na Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo yao wamejadili umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi wanachama na mahakama hizo katika kukamata watuhumiwa, kuwarejesha maeneo husika watuhumiwa waliothibitika kutokuwa na hatia au waliokamilisha vifungo vyao pamoja na umuhimu wa kuheshimu maadili na mchakato mzima wa uendeshaji wa kesi.