Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa Yemen

Ban akaribisha kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha kuanzishwa kwa mazungumzo ya kitaifa nchini Yemen, katika kongamano la siku ya kumbukumbu ya wale walokufa katika maandamano ya amani mnamo Machi 18 mwaka 2011. Katika taarifa ilotolewa na msemaji wake, Bwana Ban amesema amefurahishwa kuona kuwa mazungumzo hayo yameandaliwa kwa njia ya kina, ni ya kujenga na jumuishi.

Amesema watu wa Yemen wamechagua njia ya mazungumzo ya amani na maridhiano, na kuongeza kuwa mazungumzo hayo yanatoa nafasi ya kihistoria kwa watu wa Yemen, wakiwemo wanawake na vijana.

Ameongeza kuwa yatawapa nafasi ya kuungana kutatua mambo yanayozua utata, kujenga imani, kuhakikisha haki, kuendeleza haki za binadamu na kuchangia maendeleo ya nchi yao.

Amehahidi kuwa mshauri wake maalum kuhusu Yemen, Jamal Benomar na timu yake wataendelea kuzungumza na wadau wote katika kusaidia mazungumzo hayo ya kitaifa.