Sheria legevu zatia mashaka usalama barabarani: WHO

14 Machi 2013

Shirika la afya duniani WHO limetoa ripoti mpya inayoonyesha kuwa ni mataifa 28 tu yenye asilimia Saba ya watu wote duniani ambayo yana sheria madhubuti za usalama barabarani kwenye maeneo makuu matano ambayo ni muhimu  katika kupunguza ajali za barabarani.

Maeneo hayo ni kunywa pombe na kuendesha gari, mwendo kasi kupindukia, matumizi ya kofia kwa waendesha pikipiki, kufunga mikanda na matumizi ya viti maalum vya watoto. Ripoti hiyo inaeleza kuwa hatari ya kufa kutokana na ajali ni kubwa barani Afrika kuliko barani Ulaya.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2010 kulikuwa na vifo zaidi ya Milioni Moja nukta Mbili vilivyosababishwa na ajali za barabarani, idadi ambayo ni karibu na ile ya mwaka 2007.

Etienne Krug, ni Mkurugenzi wa Idara ya kuzuia majanga na ulemavu ndani ya WHO na anasema suluhishi ni sheria na kuzisimamia.

(SAUTI YA Krug)

"Hili ni tatizo linalosababishwa na binadamu ambalo tunaweza kupatia jawabu.tunafahamu nchi nyingi zimepata mafanikio makubwa katika miongo kadhaa na tungependa walichofanikiwa kiwe fundisho kwa wengine. Moja ya fundisho ni kwamba tunahitaji sheria nzuri kwenye maeneo makuu hatarishi.kwa hiyo ni muhimu sana kuwa na sheria nzuri na muhimu zaidi kusimamia sheria hizo. Nchi nyingi zimetueleza kuwa udhibiti wa sheria bado ni tatizo na hivyo unahitahi kuimarishwa.