Watu kutoweka katika mazingira tata bado ni tatizo duniani: De Frouville

6 Machi 2013

Mwenyekiti wa kikundi cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na udhibiti wa vitendo vya watu kutoweka katika mazingira tatanishi Olivier De Frouville amesema matukio ya watoto kutoweka katika mazingira hayo ni mojawapo ya vitendo vibaya zaidi vya ukatili dhidi ya watoto. Katika taarifa yake aliyoitoa mjini Geneva, Uswisi, De Frouville amesema kwa kuzingatia kuwa kutoweka katika mazingira tatanishi ni uhalifu unaoendelea, madhara yake kwa mtoto yanaweza kuendelea hata baada ya kuwa mtu mzima.  Amesema kikundi hicho tangu kuundwa kwake, kimeshaewasilisha kwa serikali mbali mbali duniani takribani matukio Elfu 54 ya watu kutoweka wakiwemo watoto lakini ni matukio karibu 300 tu yaliyotolewa ufafanuzi.  Amesema matukio ya watu kutoweka bado ni tatizo kubwa duniani hususan kwenye nchi zenye migogoro au vita vya wenyewe kwa wenyewe.   Kwa mujibu wa De Frouville, kutoweka kwa watoto na athari wanazopata wanawake kutokana na matukio ya watu kutoweka kwenye mazingira tata ni mambo ambayo kikundi hicho kimeshatolea taarifa maalum na kwamba inapaswa kufahamika kuwa wanawake wako mstari wa mbele katika kukabiliana na matukio ya watu kutoweka katika mazingira tatanishi.