Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yataja changamoto za kukabiliana na ukeketaji wanawake na watoto wa kike

UNFPA yataja changamoto za kukabiliana na ukeketaji wanawake na watoto wa kike

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Idadi ya watu duniani, UNFPA, Dkt. Babatunde Osotimehin amesema licha ya mafanikio katika kupambana na ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike, bado kuna changamoto kubwa kutokomeza kabisa tabia hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Radio ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Babatunde ametaja changamoto hiyo kuwa ni ajira mbadala kwa mangariba kwa kuwa hufanya kitendo hicho kwa manufaa ya kiuchumi vile vile.

 (SAUTI BABATOUNDE)

“Nafikiri tunapiga hatua nzuri, tunazungumza na waatalamu ili kuhakikisha tunawapatia ajira mbadala mangariba, na pia kuhakikisha tunaelimisha jamii juu ya madhara ya ukeketaji. Siyo tu kwamba ni kitendo dhalili bali pia ni kitendo kinachosababisha madhara kwa wanawake.”

Miongoni mwa nchi ambazo ukeketaji wanawake na watoto hufanyika ni Tanzania ambapo Mwakilishi wa kudumu wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi amesema kwa sasa kinafanyika kwa siri zaidi, na hivyo hiyo ni changamoto ndani ya mafanikio.

Balozi Manongi ametaja pia njia mbadala inayotumiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jinsia, wanawake na watoto nchini Tanzania kutokomeza ukeketaji pamoja na taarifa kuwa baadhi ya madaktari wanadaiwa kushiriki kutekeleza kitendo hicho dhalili.

(SAUTI Balozi Manongi-Mikopo)

Akizungumzia siku hii ya leo ya kutokomeza ukeketaji, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN-WOMEN Michelle Bachelet amesema shirika lake linaunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali, wananchi na taasisi mbali za kutokokomeza ukeketaji.

Amesifu hatua za jamii kwenye nchi kadhaa ikiwemo Somalia,  Benin, Burkina Faso, Ethiopia, Senegal na Misri za kupaza sauti moja na kukataa kitendo hicho kwa lengo la kulinda afya na utu wa mwanamke na mtoto wa kike.