Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umeonya juu ya mshambulizi dhidi ya shule wakati wa vita

UM umeonya juu ya mshambulizi dhidi ya shule wakati wa vita

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imesema kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya makusudi dhidi ya shule au kulazimisha shule hizo kufungwa katika maeneo yanayokabiliwa na vita duniani.

Ripoti hiyo ya kila mwaka ya mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya watoto kwenye vita imebaini kwamba kati ya migogoro 22 iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu mashambulizi dhidi ya shule na hospitali yamefanyika katika migogoro 15.

Radhika Coomaraswamy amesema uharibifu wa majengo ya shule unatokea mara kwa mara na ni ukiukaji wa sheria lakini pia kuna taarifa za shule kufungwa kwa sababu ya kutekwa na jeshi au tvitisho vya moja kwa moja.

Ripoti hiyo inasema miundombinu ya shule imesambaratishwa na wapiganaji , na wanafunzi na waalimu wameshambuliwa, kutishwa au kunyanyaswa na katika maeneo mengine shule zinalekwa makusudi hali inayowaweka wanafunzi katika hatari kubwa.

Bi Coomaraswamy amesisitiza kuwa shule wakati wote zinapaswa kuwa ni mahali salama kwa wanafunzi kusoma, hivyo zinapaswa kulindwa..