WFP yaendelea kusambaza vyakula Syria na Mali

5 Februari 2013

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema lina mpango wa kuwa limefikisha misaada kwa watu Milioni Mbili na Nusu nchini Syria ifikapo mwezi Aprili mwaka huu.

WFP imesema msaada wa chakula unajumuisha bidhaa nane ikiwemo  mchele, sukari, chumvi na kwamba tayari wamepata kibali cha kuingiza nchini humo mafuta kwa ajili ya magari pamoja na unga wa ngano.

Wakati huo huo WFP imesema imeanza kusambaza tena vyakula kwenye maeneo ya kaskazini mwa Mali  ambako ndiko mapigano yalianzia.

Elizabeth Byrs ni msemaji wa WFP.

(SAUTI YA BYRS)

WFP ilianza tena kusambaza misada maeneo ya Kaskazni tarehe 2 na 3 mwezi huu. Boti saba zikiwa na tani za ujazo 600 za vyakula ziliondoka bandari ya Mopti kwenda wilaya ya Niafunke huko Timbuktu. Msaada huo utanufaisha watu zaidi ya Elfu 34 wakiwemo watoto Elfu mbili mia Tisa Sabini wenye umri wa chini ya miaka Mitano na wanawake 610 wakiwemo wajawazito na wale wanaonyonyesha kwa lengo la kuepusha utapiamlo.